Rais John Magufuli ambaye amefanya ziara ya siku mbili nchini Namibia, ametembelea na kuweka shada la maua katika eneo la Makaburi la Mashujaa waliopigania ukombozi wa Namibia, lililopo nje kidogo ya jiji la Windhoek nchini humo.

Katika eneo hilo, wamezikwa Mashujaa wa ukombozi wa Namibia, ambao baadhi yao walipata mafunzo katika kambi ya Kongwa nchini Tanzania, wengine walikuwa maafisa wa Chama cha SWAPO ambao ofisi zao zilikuwa jijini Dar es salaam na wengine ni viongozi wakuu walioendesha mapambano wakiwa nchini Namibia.
Baadhi ya mashujaa waliozikwa katika eneo hilo ni Ndimo Hamaambo, Peter Nanyemba, Theo-Ben Gurirabo na Toiro ya Toire.

Baada ya kutembelea eneo hilo, Rais Magufuli ametembelea kiwanda cha nyama cha kampuni Meatco kilichopo jijini Windhoek na kuelezwa na Kaimu Mtendaji Mkuu wa kiwanda hicho Jannie Breytenbach kuwa kiwanda hicho kina uwezo wa kuchinja ng’ombe 630 kwa siku, kimeajiri wafanyakazi 650 na kwamba kipo tayari kushirikiana na Tanzania kuanzisha viwanda vya nyama.
Akizungumza akiwa katika kiwanda hicho cha nyama, Rais Magufuli amesema kuwa Tanzania ni nchi ya pili kwa kuwa na idadi kubwa ya mifugo Barani Afrika na ameikaribisha kampuni ya Meatco kuwekeza nchini Tanzania.
Katika ziara hiyo ya siku mbili nchini Namibia, Rais Magufuli ameongozana na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina, Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi.
Kabla ya kuondoka nchini Namibia kwenda nchini Zimbabwe ambako anakwenda kufanya ziara rasmi kwa mwaliko wa Rais Emmerson Mnangagwa, Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Mstaafu wa Pili wa Namibia, – Hifikepunye Pohamba jijini Windhoek.
