Rais John Magufuli amezitaka Taasisi za kutoa haki kutekeleza wajibu wao ipasavyo, ili kuepuka mrundikano wa mahabusu nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa jengo la mahakama ya wilaya ya Chato na uwekekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la kituo cha Zimamoto na Uokoaji katika wilaya hiyo ya Chato mkoani Geita, Rais Magufuli amelitaka Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kusaidiana na Mahakama kuhakikisha wanafanikisha suala hilo.
Amesema kuwa si jambo zuri Tanzania kuwa na Mahabusu wengi kuliko Wafungwa na kumtaka Mwendesha Mashtaka kuendelea kutembelea Magereza mbalimbali nchini na kuangalia namna ya kuwaachilia huru Mahabusu wasio na hatia.
Kwa mujibu wa Rais Magufuli, takwimu zilizopo sasa zinaonyesha Tanzania ina takribani Mahabusu Elfu 17, huku Wafungwa wakiwa takribani Elfu 12 jambo ambalo halipendezi.
Halikadhalika Rais Magufuli amesema kuwa, Serikali itaendelea kuajiri Watumishi wa mahakama, lengo likiwa ni kuharakisha mashauri mbalimbali yanayofikishwa Mahakamani.
Akizungumzia utendaji kazi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini Rais Magufuli amelitaka kuongeza juhudi utendaji kazi ili kumaliza malalamiko yanayotolewa mara kwa mara na Wananchi kuwa Jeshi hilo limekua likifanya kazi chini ya kiwango pindi yanapotokea majanga ya moto.
