Rais dkt. John Magufuli ameshuhudia utiaji saini wa mkataba wa mauziano ya mahindi kati ya wakala wa taifa wa hifadhi ya chakula (Nfra) na shirika la chakula duniani (Wfp) uliofanyika ikulu jijini Dar es salaam.
Mkataba huo umetiwa saini na kaimu mtendaji mkuu wa Nfra Vumilia Zikankuba na mwakilishi na mkurugenzi mkazi wa Wfp hapa nchini Michael Danford, ambapo Wfp itanunua tani 36,000 zenye thamani ya shilingi bilioni 21 kutoka Nfra.
Danford amesema mahindi hayo ni sehemu ya tani laki 1 na 60 elfu za chakula zenye thamani ya shilingi bilioni 132.2 zilizonunuliwa na Wfp nchini tanzania katika mwaka 2018, ikiwa ni ongezeko la kutoka shilingi bilioni 63.6 zilizotumika kununua chakula mwaka 2017.
Danford amebainisha Wfp limeamua kuwa mnunuzi mkubwa wa mazao ya chakula nchini tanzania kwa ajili ya kusaidia wakimbizi na nchi jirani zenye matatizo ya chakula.
Pamoja na kushuhudia utiaji saini wa mkataba huo Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali zikiwemo Jeshi la Polisi, Wakala wa barabara Tanzania (Tanroads), shirika la viwango Tanzania (tbs), Mamlaka ya mapato Tanzania (tra), Shirika la Reli Tanzania (trc) na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (tpa) kuhakikishia wanaondoa urasimu na kuharakisha ununuzi wa mazao yanayonunuliwa na Wfp (ili wakulima wa wanufaike na fursa hiyo.