Rais Magufuli arejea nchini

0
548

Rais John Magufuli amerejea nchini hii leo akitokea nchini Zimbabwe ambako amefanya ziara rasmi ya siku Tatu kwa mwaliko wa Rais Emmerson Mnangagwa wa nchi hiyo.

Kabla ya kufanya ziara nchini Zimbabwe, Rais Magufuli amefanya ziara nchini Afrika Kusini ambako pamoja na kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais wa awamu ya tano wa nchi hiyo Cyril Ramaphosa,  alifanya mazungumzo na kiongozi huyo Ikulu jijini Pretoria.

Baadaye,  Rais Magufuli akaelekea nchini Namibia ambako amefanya ziara ya Kitaifa kwa mwaliko wa Rais Hage Geingob wa nchi hiyo ambapo pamoja na kufanya naye mazungumzo  alifungua mtaa mkubwa uliopatiwa jina la Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na pia alitembelea eneo walipozikwa mashujaa wa ukombozi wa Namibia na kiwanda cha nyama cha Meatco.

Alipowasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam,  Rais Magufuli amepokelewa na mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, -Paul Makonda na viongozi wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama wakiongozwa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Mabeyo.