Rais Magufuli amuahidi ushirikiano Rais mpya wa Malawi

0
373

Rais John Magufuli amemtumia salamu za pongezi Rais mpya wa Malawi, Dkt. Lazarus Chakware ambaye ameibuka mshindi katika uchaguzi wa marudio uliofanyika Juni 23 mwaka huu.

Rais Magufuli ametumia salamu hizo kumhakikishia kiongozi huyo kuwa Tanzania itaendeleza uhusiano mzuri na ujirani mwema na taifa hilo la Kusini Mashariki mwa Afrika

“Kwa niaba ya Serikali na Watanzania wote naahidi kuendeleza uhusiano wetu wa kidugu, kirafiki na ujirani mwema hususani katika masuala ya uchumi na ustawi wa jamii,” ameeleza Rais Magufuli.

Chakware ametwaa nafasi hiyo baada ya kumshinda Rais Peter Mutharika ambaye alikuwa akigombea kwa muhula wa pili. Katika uchaguzi huo Chakware alipata kura 59.34% huku Mutharika akipata kura 39.92%.

Uchaguzi wa marudio ulifanyika kufuatia Mahakama ya Katiba kufuta matokeo ya uchaguzi wa Mei 2019 uliompa Rais Mutharika ushindi, kutokana na kukumbwa na kasoro nyingi.