Rais John Magufuli amesema kuwa, Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda ni miongoni mwa viongozi Wastaafu ambao wamekua wakimsaidia kuongoza nchi.
Rais Magufuli ambaye anaendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Katavi, ameyasema hayo mara baada ya kuzindua barabara ya Kanazi – Kizi – Kibaoni yenye urefu kilometa 76.6, ambapo kijiji cha Kibaoni ndipo nyumbani kwa Mzee Pinda.
“Leo ilitakiwa awe hapa Mzee Pinda, ananisaidia sana kuongoza nchi, yule baba ana moyo wa kipekee, ni mtu mwema sana na ni mtu mmoja mstaarabu sana, ndio maana nimemchagua kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)”, amesema Rais Magufuli.
Ameongea kuwa, kutokana na msaada mkubwa alionao Mzee Pinda ndio maana amemtuma akamuwakilishe katika kumbukumbu ya miaka Ishirini ya kifo cha Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere nchini China kwa kuwa aliona hana mtu mwingine atakayeweza kumuwakilisha vizuri.
Mzee Pinda ametumikia nyadhifa mbalimbali Serikali ikiwa ni pamoja na Wadhifa wa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Serikali ya awamu ya Nne.
