Rais Magufuli akutana na mjukuu wa Malkia Elizabeth II

0
2725

Rais John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na mjukuu wa Malkia Elizabeth II wa Uingereza, -Prince William Ikulu jijini Dar es Salaam.

Katika mazungumzo hayo Prince William ameelezea kufurahishwa na uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Uingereza na amemshukuru Rais Magufuli kwa kupata nafasi ya kuzungumza nae.

Prince William amezungumzia juhudi anazozifanya katika uhifadhi wa wanyamapori na amemuomba Rais Magufuli kuendelea kushirikiana nae katika kukabiliana na vitendo vya ujangili hasa wa Tembo.

Kwa upande wake Rais Magufuli amemkaribisha Prince William kuja Tanzania wakati wowote na amemuhakikishia kuwa Tanzania itaendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano wake na Uingereza hasa katika uhifadhi wa wanyamapori.

“Naomba ufikishe salamu zangu kwa Malkia Elizabeth II, mwambie Watanzania tunaipenda Uingereza na tutaendeleza na kuuimarisha zaidi ushirikiano wetu mzuri kwa manufaa yetu sote” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli ameongeza kuwa serikali ya awamu ya tano imefanya juhudi kubwa za kukabiliana na ujangili hasa wa Tembo ambapo kwa sasa umepungua kwa kiasi kikubwa na kwamba anatarajia Prince William ataunga mkono juhudi hizo ili kukomesha kabisa ujangili katika hifadhi zote za wanyamapori nchini.

Prince William atakuwa nchini kwa muda wa siku nne hadi Septemba 29 mwaka huu.