Uamuzi wa serikali wa kufungua ubalozi wa Tanzania nchini Israel umeanza kuzaa matunda, baada ya timu ya madaktari na wataalamu wa matibabu ya moyo 30 kutoka nchini Israel kuja nchini kwa lengo la kuokoa maisha ya watoto 51 wanaopatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es salaam.
Timu ya madaktari na wataalamu hao wakiwemo wawili kutoka nchi za Marekani na Canada ambao wanatoka shirika la Save a Child’s Heart la nchini Israel, wamekutana na Rais John Magufuli Ikulu jijini Dar es salaam.
Mkutano huo pia umehudhuriwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Profesa Mohamed Janabi ambaye amesema kuwa kati ya watoto 51 wanaopatiwa matibabu katika kampeni maalum, kumi watafanyiwa upasuaji wa kufungua kifua na ishirini watafanyiwa upasuaji kwa kutumia tundu dogo.
Profesa Janabi amefafanua kuwa kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita, JKCI imetoa matibabu ya moyo kwa wagonjwa 254,881 ambapo kati yake 799 wamefanyiwa upasuaji wa kufungua kifua, 2,056 wamefanyiwa upasuaji kwa kutumia tundu dogo na wengine wamepatiwa matibabu mengine ya moyo.
Ameongeza kuwa ushirikiano wa JKCI na wataalamu kutoka nje ya nchi umesaidia kuwawezesha wataalamu wa Tanzania kutoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo na pia kuokoa gharama kubwa zilizokuwa zikitumika kupeleka wagonjwa nje ya nchi, ambapo kwa kipindi cha miaka mitatu Tanzania imetumia shilingi bilioni 22 ikilinganishwa na shilingi bilioni 87.8 ambazo zingetumika kutoa matibabu hayo nje ya nchi.
Wakizungumza wakati wa mkutano huo, viongozi wa timu hiyo ya madaktari na wataalamu wa matibabu ya moyo kutoka nchini Israel wamemshukuru Rais Magufuli kwa ushirikiano mkubwa ambao wameupata kutoka serikali na wameahidi kuendelea kushirikiana na serikali ili kuokoa maisha ya watoto.
Kwa upande wake Rais Magufuli amewashukuru madaktari na wataalamu hao kwa kuja nchini kuokoa maisha ya watoto na pia amemshukuru Waziri Mkuu wa Israel, – Benjamin Netanyahu kwa kuendeleza na kuimarisha uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Israel.
Rais Magufuli amemuandikia barua ya shukrani Waziri Mkuu Netanyahu na kuikabidhi kwa balozi wa Israel nchini Noah Gal Gendler ambapo pamoja na kushukuru kwa msaada wa matibabu pia amemshukuru kwa ushirikiano katika sekta nyingine.
“Israel ni marafiki zetu wa siku nyingi, tunasaidiana na kushirikiana kwa mengi, ndio maana niliona tufungue ubalozi wetu kule Israel ili kurahisha masuala haya muhimu ya ushirikiano na yenye manufaa kwa watu wetu” amesisitiza Rais Magufuli.
Rais Magufuli amemuomba balozi huyo wa Israel nchini na wataalamu hao kuwahamasisha wawekezaji wanaoweza kujenga viwanda vya dawa na vifaa tiba nchini na kuwahakikishia kuwa serikali itanunua dawa na vifaa hivyo, na pia watakuwa na uhakika wa soko la Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).
Pia Rais Magufuli amewapongeza madaktari wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete kwa juhudi kubwa wanazozifanya katika kuokoa maisha ya Watanzania na amewahakikishia kuwa serikali inatambua juhudi hizo na itaendelea kuwajengea mazingira bora ya kazi.
Wakati huohuo, Rais Magufuli amefanya mazungumzo na balozi wa Israel nchini Noah Gal Gendler na baada ya mazungumzo hayo Gendler amesema kuwa Israel imetoa nafasi za masomo kwa Watanzania 150 watakaogharamiwa na serikali ya Israel kwa ajili ya kujifunza utaalamu wa kilimo cha kisasa kwa muda wa miezi 11.