Rais Magufuli akerwa na ucheleweshwaji wa mradi wa bomba la mafuta

0
217

Rais John Magufuli amemtaka Rais wa Yoweri Museveni wa Uganda kuwa mkali kwa Watendaji wake ambao wanakwamisha kuanza kwa mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini humo mpaka mkoani Tanga.

Akizungumza jijini Dar es salaam wakati wa kongamano la biashara kati ya Tanzania na Uganda, Rais Magufuli amesema kuwa Tanzania ilifanya mabadiliko ya sheria ili kupunguza sehemu ya kodi kwa ajili ya mradi huo.

Amemtaka pia Rais Museveni kuchukua hatua nchini kwake kwa kuwa tayari kupoteza kidogo kama Tanzania ilivyofanya ili apate kikubwa zaidi.

Pia, amemshauri kama Watendaji wake ndio kikwazo asisite kuwaondoa na kuweka wengine.

“I wish hawa watendaji wa Tanzania wangeenda Uganda na wa Uganda waje Tanzania ili ni-deal nao angalau kwa mwezi mmoja tu,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli ametolea mfano wakati alipoingia madarakani mwaka 2015 alibadilisha Makamishna Wakuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) watano, lengo likiwa ni kuongeza ufanisi katika mamlaka hiyo.

Amewataka watendaji katika nchi za Uganda na Tanzania wahakikishe wanafanikisha miradi mikubwa ambayo inatengeneza ajira nyingi na kuongeza kuwa watendaji wengi wa serikali hawajali kwa sababu wanapata mishahara.

Kwa upande wake, Rais Museveni amewataka wafanyabiashara kujadiliana kwa kina na kujibu swali linalouliza “utajiri wa mataifa unatoka wapi” kama lilivyoulizwa na Adam Smith kwenye kitabu chake cha Wealth of Nations.

Amesema kuwa, suala la miundombinu ni muhimu katika kurahisisha biashara baina ya Tanzania na Uganda kwa kuwa gharama za usafirishaji wa kontena kutoka bandari ya Dar es salaam kwenda Port Berry itakuwa Dola 1600 za Kimarekani badaka ya Dola 4500 za Kimarekani za sasa.

Rais Museveni amemuhakikishia Rais Magufuli kuwa Uganda itahakikisha bomba la mafuta linajengwa na mafuta ambayo yamekuwepo kwa miaka Milioni Mbili iliyopita yanapatikana kwa maendeleo ya wananchi.