Rais John Magufuli amekutana na viongozi wa Taasisi ya Mashauriano ya Kisheria kwa nchi za Asia na Afrika (AALCO), ambao wanahudhuria mkutano wa 58 unaofanyika hapa nchini kwa muda wa siku Tano ukiwakutanisha Wajumbe kutoka nchi Wanachama 49 na Mashirika mbalimbali.
Wakati wa mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu jijini Dar es salaam, Rais Magufuli amewashukuru na kuwakaribisha Tanzania Wajumbe wote wanaohudhuria mkutano huo na amewahakikishia kuwa Serikali inatambua kazi inayofanywa na AALCO tangu Tanzania ijiunge mwaka 1965 na kuwa Mwanachama kamili kuanzia mwaka 1973.
Rais Magufuli amesisitiza umuhimu wa Taasisi hiyo ya Mashauriano ya Kisheria kwa nchi za Asia na Afrika kutekeleza malengo yake, na ametoa wito wa kuendelea kuzitetea nchi Wanachama hasa zinazowekewa vikwazo mbalimbali, huku akitolea mfano Zimbabwe ambayo imewekewa vikwazo kwa miaka mingi.
Viongozi wa Taasisi hiyo waliokutana na Rais Magufuli ni Rais wa AALCO aliyechaguliwa katika mkutano huo unaoendelea Balozi Augustine Mahiga ambaye ni Waziri wa Sheria na Katiba, Makamu wa Rais wa AALCO aliyechaguliwa katika mkutano huo Profesa Mohamad Shalaldeh ambaye ni Waziri wa Sheria wa Palestina, Katibu Mkuu wa AALCO Profesa Kennedy Gastorn kutoka nchini Tanzania na Naibu Makatibu Wakuu wa AALCO watatu ambao ni Yukihiro Takeya kutoka Japan, Wang Liyu kutoka China na Dkt Ali Garshasbi kutoka Iran.
Rais wa AALCO Balozi Mahiga na Katibu Mkuu Profesa Gastorn, wamemshukuru Rais Magufuli kwa kupata fursa ya kukutana nae na wameahidi kuwa Taasisi hiyo itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa maslahi ya Asia na Afrika.