Rais Magufuli Aipongeza ATCL

0
313

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 14 Desemba, 2019 amewaongoza wananchi wa Mwanza na Mikoa jirani kuipokea ndege mpya aina ya Bombardier Dash 8–Q400 iliyonunuliwa na Serikali ya Tanzania na kutua kwa mara ya kwanza hapa nchini katika uwanja wa ndege wa Mwanza.

Ndege hiyo inakuwa ya 8 kuwasili hapa nchini kati ya ndege 11 zilizonunuliwa na Serikali ya Tanzania kwa lengo kuimarisha huduma za usafiri wa anga kupitia Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) na kukuza sekta ya utalii.

Sherehe za mapokezi ya ndege hiyo zimefanyika katika uwanja wa ndege wa Mwanza na kuhudhuriwa na wananchi na viongozi mbalimbali wakiwemo Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Spika wa Bunge Job Yustino Ndugai, Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Kayanza Peter Pinda, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi, Balozi wa Canada hapa nchini Pamela O’Donnell, Mawaziri na Naibu Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu, viongozi wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Wakuu wa Mikoa, Wabunge, viongozi wa Dini na viongozi wa siasa.

Katika hotuba yake, Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa kwake na mafanikio makubwa ya kuimarishwa kwa usafiri wa anga kama alivyowaahidi Watanzania wakati akiingia madarakani Novemba 2015, ambapo ATCL imeimarika kwa kuongeza idadi ya ndege kutoka 1 hadi 8, kuongeza idadi ya abiria kutoka 4,000 hadi 62,000 kwa mwezi, kuongezeka kwa mizigo kutoka tani 9 hadi 177 kwa mwezi na kwa ujumla ATCL imeongeza umiliki wa soko la ndani hadi kufikia asilimia 73.

Ameipongeza ATCL kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana ikiwa ni pamoja na kuanza kufanya matengenezo makubwa na madogo hapahapa nchini kwa ndege aina ya Bombardier Dash 8-Q400 hali iliyosadia kuokoa shilingi Milioni 590, kujijengea uwezo wa kufanya matengenezo ya ndege kubwa aina ya Airbus A220-300 na Boeing 787-8 Dreamliner ambapo wahandisi 24 wanaendelea kupata mafunzo na kuboresha karakana za ndege ambapo sasa matairi ya ndege zote yanaundwa hapahapa nchini hivyo kuokoa fedha na muda.