Rais John Magufuli amesifu utendaji kazi wa Waziri wa Viwanda na Biashara Innocent Bashungwa kwa namna alivyoshughulikia suala la ununuzi wa Korosho, ambapo tayari korosho zenye thamani ya Shilingi Bilioni 120 zimenunuliwa na zoezi hilo linaendelea kwa kasi.
Akizindua kiwanda cha Pipes Industries Company Limited jijini Dar es salaam, Rais Magufuli amesema kuwa Wizara ya Viwanda na Biashara inaendelea kupata mafanikio hasa katika kipindi kifupi ambacho Waziri Bashungwa ameisimamia.
Rais Magufuli amefafanua kuwa, Serikali iliamua kununua korosho za Wakulima msimu uliopita na tangu muda huo korosho hizo zilikuwa hazijapata mnunuzi, lakini katika kipindi kifupi ambacho Waziri Bashungwa ameiongoza wizara hiyo ametafuta soko na tayari korosho imeanza kusafirishwa nje ya nchi.
Kiwanda hicho kinachojengwa kwa awamu Sita, kitakuwa na uwezo wa kutengeneza mabomba ya aina zote, ambapo kwa sasa kinazalisha Tani Elfu 25 za mabomba kwa mwaka.