Rais John Magufuli amefanya uteuzi wa Wenyeviti wa Bodi Nne za Taasisi za Serikali na Mkuu wa Chuo mmoja.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi imeeleza kuwa, walioteuliwa ni Mhandisi Emmanuel Korosso anayekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) na Dkt Alexander Kyaruzi anayekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Wengine ni Joseph Odo Haule aliyeteuliwa na Rais Magufuli kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara na Dkt Felician Kilahama aliyeteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI).
Taarifa hiyo imeeleza kuwa, Wenyeviti hao wa Bodi wameteuliwa kushika nyadhifa hizo kwa kipindi cha Pili baada ya kipindi cha kwanza kumalizika, na uteuzi wao umeanza Novemba Tisa mwaka huu.
Rais Magufuli pia amemteua Profesa Shadrack Mwakalila kuwa Mkuu wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
Profesa Mwakalila anashika wadhifa huo kwa kipindi cha Pili na uteuzi wake umeanza Novemba Nane mwaka huu