Rais Magufuli afanya mabadiliko madogo baraza la mawaziri

0
1029

Rais Dkt. John Magufuli amefanya mabadiliko madogo katika baraza la mawaziri, kuteua makatibu wakuu, Naibu Katibu Mkuu, Balozi na Katibu Tawala wa mkoa.

Akitangaza mabadiliko hayo Ikulu jijini Dar Es Salaam Katibu Mkuu Kiongozi Dkt. John Kijazi amesema walioteuliwa ni pamoja na Angela Kairuki ambaye amekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji, Doto Biteko amekuwa Waziri wa Madini ambapo Stanslous Nyongo anaendelea kuwa Naibu Waziri wa Madini.

Katika uteuzi huo Rais Magufuli amemteua Joseph Nyamuhanga kuwa Katibu Mkuu –TAMISEMI kuchukua nafasi ya Musa Iyombe aliyestaafu kwa mujibu wa sheria.

Zainab Chaula anakuwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuchukua nafasi ya Dkt. Mpoki Ulisubisya aliyeteuliwa kuwa Balozi. Dkt. Ulisubisya atapangia baadae kituo cha kazi.Dorothy Mwaluko ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera na Uwekezaji,Elius  Mwakalinga anakuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi.

Kwa upande wa Naibu Katibu wakuu walioteuliwa ni pamoja na Dorothy Gwajima anayekwenda TAMISEMI, Dkt. Francis Michael anayekuwa Naibu Katibu Mkuu Utumishi na nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Ulinzi ikiwa imefutwa rasmi.

Aidha Profesa Faustine Kamuzora ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa mkoa wa Kagera.