Rais Magufuli aanza ziara Kagera

0
195

Rais Dkt John Magufuli amewasili mjini Bukoba mkoani Kagera ambapo hapo kesho ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa chuo cha VETA na kuzindua shule ya sekondari Ihungo ambayo imejengwa upya baada ya kuathiriwa na tetemeko la ardhi lilitokea mwezi septemba mwaka 2016.

Rais Magufuli ambaye ameongozana na Mkewe Mama Janeth Magufuli, amewasili Mjini Bukoba akitokea Chato mkoani Geita.

Akiwa safarini, Rais Magufuli amewasalimu Wananchi wa Muleba na Kemondo ambapo amewashukuru kwa kumpigia kura nyingi katika uchaguzi mkuu uliopita, kura zilizomwezesha kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi cha pili.

Amewahakikishia Wananchi hao kuwa Serikali itahakikisha ahadi zilizowekwa kwenye Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM (2020-2025) zinatekelezwa ili kuinua ustawi wa Wananchi na kukuza uchumi wa Taifa.

Rais Magufuli amezitaka taasisi na mamlaka zote zinazohusika katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara, miundombinu ya elimu, afya na maji kutekeleza wajibu wao ipasavyo na kwamba yeye atafuatilia kwa ukaribu.

Amewahakikishia Wananchi wa Muleba kuwa barabara ya Kanyambogo – Nshamba yenye urefu wa kilomita 5 itajengwa kwa kiwango cha lami, na ameagiza barabara ya Muleba – Rubya yenye urefu wa kilomita 19 ambayo imejengwa kwa kiwango cha lami iitwe barabara ya Mujungi ikiwa ni kutambua mchango mkubwa wa Marehemu Mhandisi Leopord Mjungi ambaye wakati wa uhai wake alisanifu na kusimamia ujenzi wa barabara nyingi hapa nchini.