Rais kuanza ziara ya siku tatu mkoani Mwanza

0
180

Rais Samia Suluhu Hassan Jumapili ya Juni 13, 2021 anatarajia kuwasili mkoani Mwanza na kuanza ziara ya kikazi ya siku tatu (hadi Juni 15).

Katika ziara hiyo Rais ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa reli ya kisasa ya (SGR) kutoka Mwanza hadi Isaka mkoani Shinyanga pamoja na kukagua miradi mbalimbali ya kimkakati.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza, mkuu wa mkoa huo, Mhandisi Robert Gabriel amewataka wakazi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kumlaki Rais Samia Suluhu Hassan.

Mhandisi Gabriel amesema, mara baada ya kuwasili mkoani Mwanza Rais Samia Suluhu Hassan atazindua kiwanda cha kusafisha madini ya dhahabu cha Mwanza pamoja na kufungua jengo la Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Kanda ya Mwanza.

Juni 14, Rais Samia Suluhu Hassan atakagua ujenzi wa daraja katika Ziwa Victoria eneo la Kigongo – Busisi, atazindua mradi wa maji wa Nyahiti wilayani Misungwi utakaohudumia wakazi elfu 65.

Rais atahitimisha ziara yake kwa kufanya mkutano na vijana wa mkoa wa Mwanza kwa niaba ya vijana wa Tanzania.