Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameondoka Zanzibar kuelekea Havana, Cuba, kumwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Kundi la 77 na China (G77+ China) utakaofanyika kuanzia tarehe 15 hadi 16 Septemba 2023.
Mkutano huo unalenga kukutanisha Mataifa yanayoendelea (Developing Countries) ili kujadili changamoto zinazoikabili dunia, hususan baada ya kuathiriwa na janga la UVIKO-19 na migogoro inayoendelea duniani, pamoja na vikwazo mbalimbali vya kiuchumi.
Hivyo, mkutano huo utajikita zaidi katika kutafuta njia bora za kujenga ustahimilivu kupitia maendeleo ya sayansi, teknolojia, na ubunifu ili kundi la G77 na China liweze kufikia malengo yake kwa pamoja.
Mkutano huu utaongozwa na kaulimbiu isemayo “Current Development Challenges: The Role of Science, Technology and Innovation.”
Rais Dkt. Mwinyi anatarajiwa kutoa hotuba katika mkutano huo na kuelezea vipaumbele vya Tanzania, pamoja na hatua zilizochukuliwa kukuza utafiti na kuimarisha matumizi ya sayansi, teknolojia, na ubunifu (STI) katika kuleta mapinduzi ya kiuchumi.