Rais Dkt. Mwinyi aipasha Hazina

0
270

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi ameiagiza Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango kuendelea na jukumu lake la kutafuta fedha za miradi na kuandaa utaratibu wa kuziachia wizara na taasisi za Serikali kuingia katika mikataba zenyewe.
 
Rais Dkt. Mwinyi ametoa agizo hilo Ikulu jijini Zanzibar, wakati wa mkutano wa kujadili utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa kwa mawaziri na makatibu makuu mara baada ya kuwaapisha.
 
Amesema ni lazima Hazina ikafanya kazi ya kutafuta fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali kwa ufanisi, jambo litakaloisaidia Zanzibar kuwa na miradi mbalimbali ya maendeleo.
 
“Kuanzia sasa Hazina ijikite zaidi na kazi ya kutafuta fedha za miradi mbalimbali tunayoitekeleza, na kuhakikisha mikataba inaingiwa na sekta husika”, amesisitiza Rais Dkt Mwinyi.

 Akitolea mfano wa mradi wa ZUSP, Rais Dkt Mwinyi amesema Ofisi hiyo ya Rais, Fedha na Mipango iliingia mkataba bila kuzishirikisha sekta zinazohusika, na hivyo kusababisha kuwepo na usimamizi dhaifu wakati wa utekelezaji wa mradi huo.