Flyover ya Mfugale yafunguliwa rasmi

0
2435

Rais John Magufuli amefungua daraja za juu katika makutano ya barabara za Nyerere na Mandela eneo la Tazara jijini Dar es salaam (Mfugale Flyover) ambazo zitasaidia kupunguza msongamano wa magari katika barabara hizo, ikiwemo kwenda na kutoka katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere.

Mfugale Flyover imejengwa na kampuni ya ujenzi ya Sumitomo Mitsui Construction Co. Ltd ya Japan kwa gharama ya shilingi bilioni 106.7.

Ujenzi wa Mfugale Flyover umehusisha njia nne za barabara zenye urefu wa kilomita moja, ina uwezo wa kubeba uzito wa tani 180 kwa wakati mmoja, imesanifiwa kuishi kwa miaka mia moja, ina barabara za pembeni, njia za waenda kwa miguu, mfumo wa mifereji ya maji ya mvua, taa za kuongozea magari na umezingatia mradi wa mabasi yaendayo haraka kwa kuacha eneo la mita 12 katikati ya barabara hizo.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Mhandisi Patrick Mfugale amesema kuwa ujenzi wa Mfugale Flyover umekamilika kabla ya tarehe iliyopangwa ambayo ni Oktoba 31 mwaka huu na kwamba katika juhudi za kukabiliana na msongamano wa magari serikali itajenga Flyover nyingine eneo la Chang’ombe katika makutano ya barabara ya Nyerere na Kawawa.

Kufuatia uamuzi wa Rais Magufuli kuwa Flyover ya makutano ya barabara ya Nyerere na Mandela iitwe Mfugale Flyover, Mwenyekiti wa bodi ya Usajili wa Wahandisi Mhandisi Profesa Ninatubu Lema amesoma wasifu wa Mhandisi Mfugale na kueleza kuwa ameitumikia nchi akiwa Mhandisi kwa miaka 41 ambapo katika kipindi hicho ameongoza katika kubuni na kusimamia ujenzi wa barabara kilomita 36,258 zikiwemo kilomita 9,951 za lami na amebuni na kusimamia ujenzi wa madaraja makubwa na madogo 1,400 yakiwemo madaraja makubwa ya Mkapa, Umoja, Rusumo, Kikwete, Nyerere, Magufuli na Sibiti.

Katika hotuba yake, Rais Magufuli ameishukuru Serikali ya Japan kwa kutoa mkopo nafuu wa ujenzi wa Mfugale Flyover, amewapongeza wakandarasi kwa kumaliza kazi mapema, ameipongeza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa usimamizi wake wa karibu na kwa namna ya kipekee amempongeza Mhandisi Patrick Mfugale kwa mchango wake mkubwa katika ujenzi wa Flyover hiyo, madaraja na barabara mbalimbali nchini.

Rais Magufuli ametoa wito kwa Wahandisi wengine na wataalamu mbalimbali nchini kuiga mfano wa Mhandisi Mfugale wa kutanguliza mbele maslahi ya Taifa badala ya kuwa kikwazo kwa kukosa uaminifu na uadilifu ama kutoa ushauri usio na manufaa kwa Taifa.

Amesema kuwa serikali itaendelea kutekeleza miradi ya kuboresha miundombinu ya jiji la Dar es salaam kama ilivyoahidi na kwamba pamoja na kujenga Flyover nyingine katika eneo la Chang’ombe pia itajenga Flyover katika eneo la Machinjioni, inajenga barabara za juu katika eneo la Ubungo, inajenga barabara ya njia nane kutoka Kimara jijini Dar es salaam hadi Kibaha mkoani Pwani yenye urefu wa kilomita 19.2.

Rais Magufuli ameagiza mradi mkubwa wa ujenzi wa barabara uitwao DMDP na ambao umetengewa shilingi bilioni 660 uhamishiwe kwenye Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA).

Ametoa wito kwa watumiaji wa Mfugale Flyover kuwa makini ili kuepuka ajali zisizo za lazima na ameagiza zifungwe kamera za kurekodi magari katika Flyover hiyo na nyingine zitakazojengwa jijini Dar es salaam.

Sherehe za ufunguzi wa Mfugale Flyover zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa wizara, balozi wa Japan nchini anayemaliza muda wake Masaharu Yoshida, Wabunge wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Seleman Kakoso, viongozi wa dini, viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama na viongozi wa mkoa wa Dar es salaam.

Wakati huohuo Rais Magufuli ameagana na balozi wa Japan nchini Masaharu Yoshida ambaye amemshukuru kwa ushirikiano mzuri alioupata kwa kipindi cha miaka mitatu na nusu aliyokuwepo nchini.

Masaharu Yoshida amepongeza uongozi mzuri wa Rais Magufuli na juhudi kubwa anazozifanya katika kujenga uchumi wa Tanzania na ameahidi kuwa balozi mzuri wa Tanzania.