Rais Dkt aomboleza vifo vya watu zaidi ya 40 nchini, atoa maagizo

0
608
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na mkewe Janeth Magufuli pamoja na waumini wengine wa Kanisa Katoliki wakishiriki Misa Takatifu Dominika ya 04 ya Mwaka “A” iliyofanyika katika kanisa la Mtakatifu Petro Parokia ya Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Rais Dkt Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa familia za watu 20 waliofariki wakati wakitoka katika ibada mjini Moshi, Kilimanjaro na kwa familia za watu zaidi ya 20 waliopoteza maisha kutokana na madhara ya mvua kubwa mkoani Lindi na mikoa mingine.

Watu 20 waliofariki dunia na 16 waliojeruhiwa mjini Moshi walikuwa miongoni mwa watu waliokusanyika viwanja vya Majengo kuhudhuria ibada iliyoongozwa na Mtume Boniface Mwamposa na wamefariki baada ya kukanyagwa na wenzao wakati wakitoka katika lango moja waliloelekezwa kupita ili kukanyaga mafuta hayo ya upako.

Rais Magufuli amemtaka Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro, Anna Mghwira, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi na wakuu wa mikoa mingine ambao mikoa yao imepata madhara ya watu kupoteza maisha kutokana na madhara ya mvua, kufikisha pole zake kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki walioguswa.

Rais Magufuli ametoa wito kwa watanzania wote kuchukua tahadhari katika matukio yote yenye viashiria vya hatari ikiwemo mikusanyiko mikubwa ya watu na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha na ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kusimamia ipasavyo tahadhari za kiusalama.