Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewaonya wafanyakazi wanaohusika na ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo haraka kipande cha Gerezani – Mbagala kutojihusisha na wizi wa vifaa.
Rais amewataka wafanyakazi kuwa wazalendo na kufanya kazi kwa uaminifu ili kuweza kulinda miradi kwa manufaa ya Watanzania.
Ametoa wito huo wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa awamu ya pili ya miundombinu ya mradi wa mabasi hayo, na kueleza kwamba wizi wa vifaa vinavyotumika kwenye ujenzi unarudisha nyuma maendeleo ya nchi.
Ametumia jukwaa hilo kumtaka mkandarasi na wizara ya ujenzi na uchukuzi kuhakikisha mradi huo unaosubiriwa kwa hamu kubwa ili kupunguza kero ya usafiri unakamilika kwa wakati.