Rais atuma salamu za pole kwa familia ya Ngusa Samike

0
260

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEM) Innocent Bashungwa amewasilisha salamu za pole za Rais Samia Suluhu Hassan kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Ndugu Ngusa Samike kufuatia kifo cha Baba yake mzazi Mzee Fredrick Shija Samike.

Waziri Bashungwa amewasilisha salamu hizo katika ibada ya maziko iliyofanyika Januari 25, 2022 katika Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga.

“Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amenituma kwa niaba yake na Serikali kutoa salamu za pole kwa familia na ninatoa pole kwa kaka yangu Ngusa kwa pengo kubwa la mzee wetu tulilolipata” amesema Bashungwa.

Waziri Bashungwa ametoa wito kwa ndugu jamaa na marafiki kuendelea kumuombea Mzee Samike huku akisisitiza umuhimu wa wananchi Mjini Kahama na kwingineko kujifunza na kuyaenzi maisha ya mzee Samike.

Mzee Fredrick Shija Samike alifariki tarehe 20 Januari 2022 katika hospitali ya Bugando iliyopo Jijini Mwanza alipokuwa akipatiwa matibabu na mwili wake umepumzishwa nyumbani kwake Kahama.