Rais akemea wanaoharibu miundombinu

0
142

Rais Samia Suluhu Hassan amekemea tabia ya baadhi ya watu wanaofanya uharibifu wa miundombinu ya barabara ikiwa ni pamoja na kung’oa alama mbalimbali na kuiba taa.

Amesema uharibifu na wizi huo umekuwa ukichangia ongezeko la ajali na kusababisha vifo na majeruhi kwa watumiaji wa miundombinu hiyo.

Rais Samia Suluhu Hassan ameyasema hayo mkoani Tabora mara baada ya uzinduzi wa barabara ya Nyahua hadi Chanya yenye urefu wa kilomita 85.4.

Amewataka wananchi wanaoishi pembezoni mwa barabara hiyo na watumiaji wengine kuitunza ili idumu na hivyo kunufaisha kizazi cha sasa na kijacho.

Aidha Rais Samia Suluhu Hassan amesema serikali ya awamu ya sita imeendeleza miradi yote iliyoanza kutekelezwa katika awamu ya tano na anafurahi kuona mingine imekamilika na kuanza kutumika.

“Ndugu zangu wananchi mimi nilikuwa makamu wa Rais awamu ya tano na miradi mingi tulianzisha na awamu hii ya sita imeendeleza na itaendelea kujengwa miradi mingine kwa ajili ya kurahisisha shughuli za uzalishaji na kuunganisha maeneo mengi pamoja na nje ya nchi” ameongeza Rais Samia Suluhu Hassan

Pia amesema serikali itaendelea kutatua changamoto za wananchi katika sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja afya na elimu kadri hali ya uchumi itakavyoruhusu.