Rais akabidhi mashuka 200 Mwananyamala

0
272

Serikali imeahidi kufanya kila linalowezekana, ili kuboresha huduma za matibabu kwa Watanzania wote.

Ahadi hiyo imetolewa mkoani Dar es salaam na Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa ziara yake katika hospitali ya rufaa ya mkoa ya Mwananyamala, ambapo pia ametoa mashuka 200 yatakayotumiwa na Wagonjwa wanaolazwa hospitalini hapo.

Akizungumza na Watumishi wa hospitali hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan amewataka kufanya kazi kwa bidii katika kuwahudumia Wananchi na kuwapatia huduma stahiki.

Amesema kwa upande wa Serikali, itahakikisha inaboresha maslahi ya Watumishi hao, pindi hali ya uchumi wa Taifa itakapokuwa nzuri.

Akiwa hospitalini hapo, Rais Samia Suluhu Hassan ameeleza kuridhishwa na utoaji huduma pamoja na usafi katika maeneo mbalimbali ya hospitali hiyo, ikiwemo wodi ya akina Mama wanaojifungua.

Ameahidi kushughulikia changamoto ya upungufu wa dawa kufuatia malalamiko aliyopatiwa na Wagonjwa wanaotibiwa katika hospitali hiyo ya Rufaa ya mkoa wa Mwananyamala.

Rais Samia Suluhu Hassan ametumia ziara yake hiyo, kuwataka Watanzania kujihadhari na ugonjwa wa corona na kuchukua tahadhari zote za kujikinga na ugonjwa huo.