Rais akaa meza moja na TPSF

0
152

Rais Samia Suluhu Hassan, leo amekutana na kufanya mazungumzo na Viongozi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).

Mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu jijini Dar es salaam, yamehusu masuala mbalimbali yanayohusu kukuza biashara na uwekezaji nchini pamoja na kupanua uwigo wa kodi.
 
Wakati wa mazungumzo hayo, Viongozi hao wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa hatua alizoanza kuchukua kuimarisha uhusiano kati ya Serikali na sekta binafsi.

Akizungimza wakati wa mkutano huo, Mwenyekiti wa TPSF Angelina Ngalula amesema sekta binafsi imeanza kuona matokeo ya juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan, ambapo kufuatia ziara yake ya nchini Kenya sekta binafsi ya nchini humo na ya Tanzania wamekubaliana kuanzisha soko la pamoja la bidhaa ambalo litawawezesha Wafanyabiashara wa pande zote kuuza na kununua bidhaa sokoni hapo.

Hata hivyo, Viongozi hao wameiomba Serikali kuendelea kutilia mkazo juhudi za kuboresha mazingira ya kufanya biashara, kusimamia ulipaji wa kodi, kusimamia manufaa ya ndani katika miradi mikubwa, kufanya utafiti, kuvutia mitaji, uwekezaji katika maeneo ya kimkakati na kutilia mkazo sekta ya kilimo ambayo inaajiri Watanzania wengi.

Kwa upande wake Rais Samia Suluhu Hassan amewapongeza Viongozi hao kwa juhudi kubwa zinazofanywa na TPSF kuitikia wito wake wa kutekeleza jukumu la kukuza uchumi na kuwahakikishia kuwaunga mkono.

Rais Samia Suluhu Hassan ameahidi kufanyia kazi maoni yao pamoja na maoni mengine yatakayotolewa katika mkutano wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), unaotarajiwa kufanyika mwezi Juni mwaka huu.