Rais Samia Suluhu Hassan ameiagiza wizara ya Maji kutoa shilingi milioni 500 kwa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira mkoani Mwanza (MWAUWASA) ili wawasambazie maji wananchi wa maeno ya Kyaka na Bunazi mkoani Kagera ambao wamepatiwa mradi mkubwa wa maji safi hii leo.
Akihutubia wananchi wa maeneo hayo, Rais Samia amesema baada ya kuzindua mradi huo wananchi hasa akina mama wangependa kuona maji yanatoka majumbani mwao na si vinginevyo na kuiagiza wizara ya Maji kutoa fedha kwa ajili ya kuunganisha maji kwa wananchi.
“Naiagiza wizara ya Maji kutoa fedha kwa mkopo, shilingi milioni 500 na muwape MWAUWASA ili wasambaze maji kwa wananchi wanaonufaika na mradi huu.” amesema Rais Samia
Aidha amewataka wananchi hao kulipa bili za maji ili kuufanya mradi huo kuwa endelevu kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
Awali akimkaribisha Rais, Waziri wa Maji Jumaa aweso amesema mradi huo umesimamiwa na wahandisi wazawa na utahudumia wananchi wa Kyaka na Bunazi wilayani Misenyi mkoani Kagera.
Mradi huo umeigharimu serikali zaidi ya shilingi bilioni 15.7 na utahudumia wananchi elfu 65.