Raia wanane wa kigeni washikiliwa na polisi Mara

0
2931

Polisi mkoani Mara inawashikilia wafanyakazi wanane raia wa Russia na Armenia kwa tuhuma za kufanya kazi nchini bila ya vibali huku kampuni inayomiliki mgodi wa MMG Musoma Vijijini ikituhumiwa kunyayasa wafanyakazi.

Tukio hilo limejiri kufuatia ziara ya ghafla ya Naibu Waziri wa Madini Dotto Biteko katika mgodi huo.

Katika tukio hilo raia hao wa kigeni wasiokuwa na vibali wamekutwa wamefungiwa vyumbani huku baadhi ya wafanyakazi wakiwa wamefungiwa vyooni.

Katika ziara hiyo Naibu Waziri Biteko amekagua maeneo mbalimbali ya mgodi huo na kuzungumza na wafanyakazi ambapo amebaini ukiukwaji wa sheria, kanuni na taratibu za uwekezaji.

Kampuni hiyo ya MMG iliwafungia vyumbani wafanyakazi wa kigeni wasiokuwa na vibali vya kufanyakazi na vibarua waliokuwa hawana vifaa vya kufanyia kazi walifungiwa chooni.

Naibu Waziri wa Madini Dotto Biteko ameiagiza kampuni hiyo ya MMG kuhakikisha inawapatia wafanyakazi wake mikataba ya ajira ndani ya siku saba.