Rada Mbili zazinduliwa JNIA

0
187

Rais John Magufuli amesema kuwa kuzinduliwa kwa Rada Mbili kwa ajili ya kuongoza ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) uliopo jijini Dar es salaam, kutaisaidia serikali kuokoa Mamilioni ya fedha yaliyokua yakitumika kuilipa nchi jirani ya Kenya, iliyokua ikilinda asilimia 75 ya anga la Tanzania.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Rais Magufuli amesema kuwa Tanzania imekua ikiilipa serikali ya Kenya fedha kwa muda wa miaka 41 baada ya Shirika la Anga Duniani (ICAO) kuipa jukumu la kulinda anga la Ukanda wa Afrika Mashariki linalojumuisha nchi za Tanzania, Madagascar, Mauritius, Comoro na Visiwa vya Mayotte.

Amesema kuwa kuzinduliwa kwa Rada hizo kutaifanya Tanzania kuwa na uwezo wa kulinda anga lake lote tofauti na ilivyokua hapo awali wa kulinda baadhi ya maeneo, kutokana na kukosa Rada zenye uwezo unaokubalika Kimataifa.

Uzinduzi huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Dini, Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wabunge, Viongozi wa vyama vya siasa, Mabalozi mbalimbali wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini  na Watendaji mbalimbali serikali.