Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Mhandisi Charles Sangweni amesema Serikali inaandaa mazingira wezeshi kwa kuelimisha kampuni zinazotarajia kutoa huduma katika mradi mkubwa wa kimkakati wa kuzalisha gesi asilia kuwa kimiminika (LNG) kusudi zizalishe kalingana na viwango vinavyohitajika kimataifa.
Akizungumza katika viwanja vya sabasaba yanapoendelea maonesho ya biashara kimataifa ya Dar es Salaam, Sangweni amesema ili kuzichangamikia fursa za uwekezaji za mradi wa kuzalisha gesi asilia LNG ni muhimu kuzingatia viwango vya kimataifa vya malighafi zinazotakiwa kutumika na bidhaa zinazotakiwa kuzalishwa ili kufikia viwango stahiki.
Ameshauri sekta mbalimbali nchini kujikita katika kuuelewa mradi na matakwa yake na kueleza kuwa hivi sasa Tanzania imepiga hatua kubwa kutokana na kuwa na kwani wataalamu wengi wa kuzalisha mafuta na gesi.
Ameongeza kuwa ujenzi wa mradi huo unatarajiwa kuanza 2025 na utagharimu takribani miaka minne hadi mitano kukamilika hivyo hadi kufika 2030 gesi asilia ya kimiminika ya kwanza inatarajiwa kuanza kuzalishwa nchini endapo hakutakuwa na kikwazo chochote.