Puma kuendelea kutoa elimu ya usalama Barabarani

0
236

Kampuni ya Puma Energy Tanzania kwa mara nyingine tena imetoa zawadi kwa Wanafunzi wa shule mbalimbali za msingi huko Zanzibar, waliofanya vizuri katika shindano la kuchora kuhusu masuala ya  usalama barabarani.

Katika shindano hilo ambapo kampuni ya Puma Energy Tanzania alikua mdhamini pekee,  Wanafunzi Watatu kati ya Ishirini wameibuka washindi  na kupatiwa zawadi.

Mshindi wa kwanza Raya Hemed kutoka shule ya msingi Mkunazini amepatiwa zawadi ya  Shilingi Laki Tano na shule yake imepatiwa Shilingi Milioni Nne.

Salum Khatib ni mshindi wa pili  kutoka shule ya msingi Kisiwandui, ambaye amepata zawadi ya Shilingi Laki Tatu, huku  mshindi wa tatu akiwa Ariff Kassim kutoka shule ya msingi ya Nyerere ambaye amekabidhiwa kitita cha Shilingi Laki Moja na Nusu.

Zawadi nyingine walizopatiwa washindi hao Watatu kutoka kampuni hiyo ya Puma Energy Tanzania  ni  mabegi ya shule, madaftari pamoja  na kalenda za hadi mwaka 2020.

Raya Hemed Mshindi wa Kwanza

Hafla ya kukabidhiwa zawadi hizo imefanyika katika shule ya msingi Kisiwandui iliyopo katikati ya Manispaa ya Zanzibar na mgeni rasmi alikua ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi  Hamad Yussuf Masauni ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani.

Meneja Mkuu wa Kampuni ya Puma Energy, – Dominic Dhanah naye alihudhuria hafla hiyo ambapo kampuni hiyo imeahidi kuendelea kusaidia jamii nchini hasa katika kutoa elimu ya Usalama barabarani kwa Wanafunzi wa shule za msingi.