Prof. Kusiluka : Wanafunzi wanamaliza hela kwenye kubeti

0
127

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Profesa Lughano Kusiluka amesema kundi kubwa la Wanafunzi linamaliza hela ya ada kwenye kamari na kuhangaika kwenye kulipa ada hadi wiki ya mwisho ya mitihani ambapo kisheria wanapaswa kufukuzwa.

Profesa Kusikula amesema hayo wakati akichangia mada kwenye Kongamano la Mapambano dhidi ya Rushwa linalofanyika jijini Arusha na kuongeza kuwa Wanafunzi wengi wanaonekana kuonewa vyuoni lakini kiuhalisia pesa wanazitumia kwenye kamari na starehe nyingine na zikishamalizika wanatafuta namna ya kuonekana hawana hatia.

“Mwanafunzi anapewa mkopo na Serikali, akipokea ile pesa anabeti, anafanya starehe mbalimbali, hela ikianza kumalizika utaona anapika bwenini na wanajua tumekataza kupika bwenini, pesa ikiisha kabisa anakuja ofisini na kuanza kulia akisema ni mtoto wa Mkulima, kumbuka huyu anayejiita mtoto wa Mkulima amepewa hela na Serikali ya kujikimu”. Amesema Profesa Kusiluka

Ameongeza kuwa wengine wanapokwenda ofisini kwake analazimika kupiga simu kwa wazazi wake na kugundua kuwa walipewa ada ya kulipa lakini hawajalipa.

“Ukichukua hatua ya kumpigia mzazi anakwambia kabisa nimempa ada, sasa changamoto mimi pale nipo makao makuu, Wabunge na wa viongozi wengine wako pale, unaweza ukasikia Wanafunzi kadhaa wakataliwa kufanya mtithani lakini hawajui nyuma ya pazia nini kimetokea, mwanafunzi huyo huyo akiona ubao umeharibika anaanza kuitisha maandamano”. Ameongeza Profesa Kusiluka

Amesema hayo ndio yanasababisha Wanafunzi wengi kuingia kwenye vitendo vya rushwa hasa watoto wa kike kujihusisha na rushwa ya ngono ili waweze kupata ada.