Katibu Mkuu wa wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Profesa Godius Kahyarara amesema serikali imedhamiria kuiona Tanzania inakuwa lango la uchumi wa Bara la Afrika kwa kuwa na viwanda vikubwa ambavyo vitasaidia kupeleka bidhaa kwenye soko la Afrika, kuongeza ajira na pato la Taifa.
Profesa Kahyarara pia amewakaribisha Wawekezaji kuwekeza katika sekta mbalimbali za kipaumbele nchini hususani sekta ya viwanda, utalii, nishati, uvuvi, usafirishaji (Reli, Anga na Majini) na uchumi wa buluu.
Ameyasema hayo alipokuwa akifungua kongamano la wawekezaji, wauzaji na wanunuaji lililofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es salaam kama sehemu ya maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yaliyoanza Juni 28 mwaka huu na yatakayofikia tamati tarehe 13 mwezi huu.
Profesa Kahyarara amewashauri wawekezaji wawekeze Tanzania kwa kuwa iko mahali pazuri kijiografia kwa kuwa na bahari inayowezesha usafirishaji wa mizigo, rasilimali za kutosha na reli ya Kisasa inayoiunganisha na masoko ya ndani na nje ya nchi kupitia bandari.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya kuendeleza Biashara Tanzania (TANTRADE) Latifa Mohammed Khamis amesema kupitia kongamano hilo kuna baadhi ya makubalino ya kibiashara yatafikiwa ili kuhakikisha fursa walizokuja nazo wawekezaji kupitia maonesho ya Sabasaba zinawanufaisha watanzania.