Polisi yasema mpaka wa Namanga ni shwari

0
124

Jeshi la polisi mkoani Arusha limewahakikishia wakazi wa mkoa huo kuwa hali ya usalama katika mpaka wa Namanga uliopo wilayani Longido ni shwari.

Kauli hiyo imetolewa na kamanda wa polisi wa mkoa wa Arusha, Justine Masejo alipotembelea mpaka huo kutokana na kuwepo kwa foleni kubwa ya malori yanayosubiri kufanyiwa ukaguzi.

Amesema hali ya usalama katika mpaka huo ni shwari na hakuna mgomo wowote wa madereva na hawatasita kuwachukulia hatua watu wachache ambao watajaribu kuhatarisha hali ya amani katika eneo hilo.

Kwa upande wake Audax Asheri ambaye ni afisa mfawidhi wa mpaka wa Namanga amesema, wanashirikiana na wenzao wa upande wa Kenya kuhakikisha wanaweka mazingira mazuri ili magari yapite vizuri na kuondoa foleni ambayo ipo katika mpaka huo.

Chama cha Wasafirishaji wa Malori Tanzania kimesema foleni hiyo inasababishwa na skana ambayo inatumika kukagua magari upande Kenya kuelemewa na wingi wa malori, na hivyo kimeiomba serikali za Tanzania na Kenya kujadiliana kuona jinsi ya kuboresha ukaguzi wa malori.