Rais Dkt. John Magufuli leo ameweka jiwe la msingi la Kiwanda cha Ushonaji Bohari Kuu ya Jeshi la Polisi na amefungua majengo ya ofisi, madarasa na bweni la wanafunzi katika Chuo cha Taaluma ya Polisi vilivyopo Kurasini katika Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam.
Kiwanda cha ushonaji ambacho kitawekwa vyerahani 200 kitakuwa na uwezo wa kuzalisha sare za askari polisi 800 kwa siku na kinatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Machi 2021 kwa gharama ya shilingi milioni 666.4.
Jengo la ofisi na madarasa na jengo la bweni lenye ghorofa 5 yamejengwa kwa gharama ya shilingi milioni 799.6 ambapo kati ya fedha hizo shilingi milioni 700 zilitolewa na Rais Magufuli alipotembelea chuo hicho mwaka 2018.
Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Simon Sirro amesema katika awamu ya pili wanatarajia kujenga jengo la ofisi la ghorofa 5 kwa gharama ya shilingi milioni 670 na bweni la ghorofa 6 kwa gharama ya shilingi Milioni 690 ili kukiboresha zaidi chuo hicho ambacho kilijengwa tangu mwaka 1958.
Amebainisha kuwa uboreshaji wa miundombinu ya chuo hicho uliofanywa kati ya mwaka 2015 na sasa umekiwezesha kuongeza uwezo wa kuchukua wanafunzi kutoka 440 hadi kufikia 625.
Akizungumza na maafisa na askari polisi katika uwanja wa Polisi Kurasini, Rais Magufuli amelipongeza jeshi hilo kwa kazi nzuriinayofanywa na Askari katika ulinzi wa raia na mali zao na amewahakikishia kuwa Serikali itaendelea kuboresha maslahi yao pamoja na kuboresha mazingira yao ya kazi.