Polisi waagizwa kuwakamata wanaofunga ving’ora na vimulimuli kwenye magari

0
470

Jeshi la Polisi Tanzania limewaagiza makamanda wa polisi wa mikoa na wakuu wa usalama barabarani kuendelea kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria wale wote wanaokiuka sheria ya matumizi ya ving’ora.

Taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime ameagiza kuchukuliwa kwa hatua za kisheria kwa wanaofunga ving’ora, vimulimuli, taa zenye mwanga mkali na taa zenye kuwakawaka kwa kubadilisha rangi ambao sheria haijawapa kibali cha kufanya hivyo na hawana vibali kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali.

Jeshi hilo limeeleza kuwa kwa mujibu wa sheria wanaoruhusiwa kufunga ving’ora na vimulimuli ni magari ya dharura ambayo ni ya polisi, majeshi, magari ya kubeba wagonjwa au magari mengine na matela ambayo yamepata kibali kutoka wizara yenye dhamana.

Magari mengine ni yale yanayotumiwa na viongozi wakuu wa kitaifa na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, hivyo kwa yeyote ambaye hayupo kwenye makundi hayo anakiuka sheria akiweka chochote kati ya vilivyoelezwa.