Polisi kuchunguza matukio ya ajali kwa Wanahabari

0
133

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye ameliagiza Jeshi la Polisi Nchini kuchambua matukio yote ya ajali za barabarani kwenye misafara ya Viongozi ambayo yamekuwa yakisababisha vifo vya Waandishi wa habari, ili kama kuna tatizo liweze kushughulikiwa.

Waziri Nape ametoa agizo hilo mkoani Mwanza, alipowaongoza ndugu, jamaa na marafiki kuaga miili ya Waandishi wa habari waliofariki dunia kwenye ajali ya gari iliyotokea tarehe 11 mwezi huu wilayani Busega mkoani Simiyu na kusababisha vifo vya watu 14, watano wakiwa ni Waandishi wa habari.

Amewaeleza waombolezaji kuwa, Viongozi wa ngazi ya juu wamemuelekeza afuatilie matukio ya ajali za magari kwenye misafara ya Viongozi, ambapo mara nyingi waathirika ni Waandishi wa habari.

Waziri Nape amesema baada ya kukabidhiwa taarifa ya uchunguzi ndipo mambo mengine yatafuata ikiwemo kubadilisha utaratibu wa safari za Waandishi wa habari kwenye misafara ya Viongozi.

Kwa mujibu wa Waziri Nape, utaandaliwa utaratibu maalum au itifaki rasmi ya namna bora ya ushiriki wa Waandishi wa habari kwenye ziara hizo za Viongozi.