Polisi Kanda Maalum Dar wasitisha kumhoji Lissu

0
272

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesitisha kumuita mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu kwa ajili ya mahojiano kama ilivyoripotiwa kwa barua na Mkuu wa Upelelezi wa Kanda hiyo, SACP Camilius Wambura.

Kupitia mkutano na waandishi wa habari Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, SACP Lazaro Mambosasa, amesema jeshi hilo limesitisha wito huo na kumtaka Tundu Lissu kuendelea na ratiba zake za kampeni za uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika tarehe 28 Oktoba, 2020.

“Tumeona ni busara kumuacha Tundu Lissu aendelee na kampeni zake na kama alivyoamrisha inspekta jenerali kuwa aripoti kituo cha polisi kule Moshi lakini hakufanya hivyo na mpaka jana usiku tulipata taarifa kuwa amefika Dar, kwa hiyo tulitaka ahojiwe na maelezo tuyapeleke kwa wenzetu Moshi,” amesema Mambosasa.

Kamanda Mambosasa amesema baada ya kutafakari kwa kina wameona ni busara wasitishe ili kumuwezesha Tundu Lissu kuendelea na kampeni lakini ataitwa na kuhojiwa kwa wakati ambao hautaathiri ratiba ya kampeni zake.

Aidha, jeshi la polisi limewataka wananchi wa Dar es Salaam kutoshiriki kwenye vitendo vya uvunjifu wa amani kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu kwani jeshi hilo limejipanga na halitamfumbia macho yeyote atakayekiuka sheria za nchi.