Pinda awataka wataalamu wa mifugo kuishauri serikali kuboresha sekta ya mifugo

0
177

Wataalamu wa uzalishaji na uendelezaji wa Mifugo na Uvuvi nchini, wametakiwa kutumia taaluma zao kuishauri Serikali namna bora ya kuboresha na kuendeleza sekta ya mifugo na uvuvi ili ziweze kutoa mchango wa kutosha katika kukuza uchumi wa nchi na kuongeza pato la taifa na uchumi wa mtu mmoja mmoja.

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu (Mst), Mizengo Pinda kwa wataalamu wa Uzalishaji na Uendelezaji wa Mifugo na Uvuvi waliotembelea nyumbani kwake jijini Dodoma, kwa lengo la kujifunza na kubadilishana utaalamu kuhusu masuala ya ufugaji, uvuvi na kilimo.

Amesema kuwa takwimu zinaonesha kuwa nchini kuna Ng’ombe wengi zaidi ya milioni 30, Mbuzi zaidi ya milioni 20 na mifugo mingine mbalimbali vyote hivyo kama vikisimamiwa vizuri, vinaweza kusaidia kukwamua wananchi kutoka katika lindi la umasikini hasa ikizingatiwa watu wengi wanaojishughulisha na ufugaji ni wafugaji wadogowadogo ambao vilevile ndio wakulima katika maeneo ya vijijini.

“Kwa hili lazima niseme ukweli bado panahitajika kazi kubwa sana, lakini napata faraja kwa sababu Rais wetu John Pombe Magufuli katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya 2020/ 2025 unaona dhamira ipo kubwa ya namna ya kuleta mabadiliko makubwa kwenye sekta ya mifugo, uvuvi na kilimo hivyo nyie Wataamu nadhani ndio kipindi muafaka sasa kwa kusaidia nchi kimawazo,” amesema Pinda

Aidha, amesema kuwa anatamani sana wataalamu hao wakaweka mifumo mizuri ya kuwavuta vijana wanaomaliza elimu zao kujiingiza katika sekta ya ufugaji, uvuvi na kilimo ili waweze kupata nafasi ya kutambua kwamba sekta hizi ni fursa kubwa inayoweza kuleta mabadiliko makubwa sana katika uchumi wa nchi na mwananchi mmoja mmoja.

Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Wataamu wa Mifugo Tanzania (TSAP), Dkt. Daniel Komwihangilo amesema wao kama wataalamu wa mifugo na uvuvi wamefaidika sana na ziara hiyo na wameweza kuona kwamba kumbe mambo yanawezekana kinachohitajika ni juhudi na uvumilivu katika kuanzisha jambo lolote.

Wataalamu hao wa mifugo wamekutana jijini Dodoma katika Kongamano la siku 3 kuanzia Disema 2- 4, 2020 kwa lengo la kujadiliana namna bora ya kuinua viwango vya minyororo ya thamani ya mifugo na uvuvi ili sekta hizo ziweze kuwa na tija kubwa kwa nchi.