PEPFAR yapunguza maambukizi mapya ya VVU

0
170

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema  Tanzania imefanikiwa kupunguza maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi kwa asilimia 58 kutoka watu 130,000 mwaka 2003 hadi watu elfu 54 mwaka 2021 kupitia Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Ukimwi (PEPFAR).

Amesema kupitia mfuko huo ambao umeleta mabadiliko makubwa katika katika mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi, vifo vinavyotokana na Ukimwi vimepungua kwa asilimia 76 kutoka 120,000 mwaka 2003 hadi elfu 29 mwaka 2021.

Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo mkoani Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya miaka 20 ya mafanikio katika mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI yaliyowezeshwa na Mfuko huo wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI.

Amesema Tanzania itaendelea kuunga mkono mpango huo katika kujenga miundombinu ya afya, kutoa mafunzo, kutoa vifaa vya uchunguzi na vifaa vya kinga binafsi, na kuanzisha mifumo ya kufuatilia maambukizi ya VVU.

“Serikali ya Tanzania inafahamu kwamba Serikali ya Marekani ni mshirika mkubwa katika kukabiliana na Virusi vya Ukimwi nchini Tanzania, ikiwa imewekeza zaidi ya dola za Marekani bilioni 6.6 kwa ajili ya kukabiliana na janga hilo.” amesema Waziri Mkuu

Kwa sasa PEPFAR inasaidia zaidi ya watu milioni 1.5 wanaoishi na VVU (WAVIU) kwenye matibabu kupitia mpango wa kuokoa maisha wa ARVs ambapo kabla ya kuanzishwa kwa mpango huo WAVIU wasiozidi elfu moja ndio walikuwa kwenye tiba ya Kupambana na Virusi vya Ukimwi.