Pato la kila mtanzania Shilingi Milioni 2.8

0
105

Wizara ya Fedha na Mipango imesema hadi kufikia Aprili 2023, Pato ghafi la Taifa (kwa bei za mwaka husika) lilikuwa shilingi Trilioni 170.3 ikilinganishwa na shilingi Trilioni 156.4 mwaka 2021.

Akiwasilisha taarifa ya Hali ya Uchumi kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa mwaka 2023/2024 bungeni jijini Dodoma Waziri wa wizara hiyo Dkt. Mwigulu Nchemba amesema, hadi kufikia Aprili 2023 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, idadi ya watu Tanzania Bara ilikuwa 59,851,347 ikilinganishwa na makadirio ya idadi ya watu 57,724,380 mwaka 2021.

Hivyo, Pato la Taifa kwa Mtu (GDP per capita) kwa mwaka 2022 lilikuwa shilingi Milioni 2.8 ikilinganishwa na shilingi Milioni 2.7 mwaka 2021, sawa na ongezeko la asilimia 5.0.

Kiasi hicho ni sawa na Dola za Kimarekani 1,229.1 mwaka 2022 kwa mtu kwa mwaka ikilinganishwa na Dola za Kimarekani 1,173.3 mwaka 2021.

Hali hii inaendelea kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ngazi ya chini.