Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan amekitaka Chuo Kikuu Huria cha
Tanzania (OUT), kuwaandaa Wanafunzi kimkakati kushiriki moja kwa moja katika
uchumi wa Viwanda pindi wanapohitimu masomo yao.
Makamu wa Rais ameeleza hayo jijini Dar es salaam, katika kilele cha
maadhimisho ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Chuo Kikuu hicho Huria cha Tanzania.
Amefafanua kuwa, lengo la Serikali katika ujenzi wa uchumi wa Viwanda, ni kuleta
maendeleo jumuishi na endelevu kwa kutumia rasilimali zinazopatikana nchini na kuongeza ajira.
Amesema Serikali inatambua umuhimu wa Sekta ya Elimu kwa maendeleo ya uchumi wa Viwanda, ndio maana inaendelea kuondoa changamoto kadhaa zinazoikabili sekta hiyo zikiwemo zile za Chuo Kikuu hicho.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda amesema kuwa, chuo hicho kimekua kikitoa Wahitimu wenye mchango mkubwa kwa maendeleo ya Taifa.
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, ndio Chuo Kikuu Huria pekee katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Kilianzishwa mwaka 1994 kikiwa na Wanafunzi Wanane, lakini kwa sasa maelfu ya Wanafunzi wamekua wakihitimu kila mwaka.