Othodox kujenga hospitali na shule

0
503

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi amekutana na kufanya mazungumzo na Kiongozi Mkuu wa Madhehebu ya Othodox Afrika, -Papa Beatitude Theodoros II jijini Dar es salaam ambaye ameelezea azma ya kanisa hilo ya kujenga hospitali na shule kubwa mkoani Dodoma.

Papa Theodoros II ameongeza kuwa,  hivi sasa Kanisa hilo linaendesha miradi mbalimbali hapa nchini ikiwa ni pamoja na kusomesha watoto wa Kitanzania wanaotoka katika familia duni mkoani Iringa ambao ni zaidi ya Elfu Nane.

Amemuomba Waziri Kabudi kusaidia jitihada za kanisa hilo la Othodox Afrika za kutaka kupata usajili wa kudumu hapa nchini pamoja na kumtaka kufikisha salamu za pongezi kwa Rais John Magufuli kutokana na jitihada anazozifanya kupitia serikali yake ya kupambana na rushwa,kuongeza uwajibikaji katika ofisi za umma na kulinda rasilimali za nchi.

Kwa upande wake Waziri Kabudi amemshukuru Kiongozi huyo Mkuu wa Madhehebu ya Othodox  Afrika kwa kumtembelea na kuongeza kuwa Tanzania licha ya kuwa na madhehebu mengi,  lakini wananchi wake wanaishi kwa kuheshimiana bila ya ubaguzi wa kidini, jambo ambalo linajenga udugu na mshikamano na kuifanya Tanzania kuendelea kuwa Taifa lenye amani.

 Amemtaka Kiongozi huyo Mkuu wa Madhehebu ya Othodox Afrika, Papa Beatitude Theodoros II kuendelea kutimiza lengo kuu la kanisa hilo la kuendeleza amani, upendo na mshikamano kwa Watanzania wote na kuhakikisha wanapiga hatua zaidi za maendeleo kupitia miradi inayofadhiliwa na kanisa hilo.