Orodha ya wanaohama ngorongoro hadharani

0
140

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amepokea orodha ya majina ya awali ya kaya 86 zenye watu 453 ambao wamekubali kuondoka kwenye hifadhi ya Ngorongoro kwa hiari.
 
Hatua hiyo ni utekelezaji wa mazungumzo ambayo Waziri Mkuu aliyafanya na Wadau wa uhifadhi kwenye vikao vilivyofanyika mwezi Februari mwaka huu kwenye tarafa za Loliondo na Ngorongoro wilayani Ngorongoro mkoani Arusha.
 
Waziri Mkuu amepokea majina hayo mara baada ya kumaliza kikao na Viongozi wa kimila wa jamii ya Kimasai (Laigwanak)
 
Akikabidhi orodha hiyo kwa Waziri Mkuu, mkuu wa mkoa wa Arusha, John Mongella amesema majina hayo ni ya awali na tayari yalishahakikiwa mara baada ya wakazi hao kujiandikisha.

“Tutawasimamia vizuri hadi waende kule wapate hati za mashamba, nyumba na maeneo ya kulisha mifugo yao.” amesema Mongella
 
Akizungumza na Malaigwanak hao zaidi ya 350, Waziri Mkuu Majaliwa amesema Rais Samia Suluhu Hassan alipofanya ziara mkoani Arusha alisema iko hatari ya kutoweka kwa hifadhi ya Ngorongoro ndani ya muda mfupi na akatoa maagizo Viongozi waende kuwasikiliza Wananchi juu ya hatua za kuchukua ili tunu hiyo isipotee.
 
“Ile hatari aliyosema Mheshimiwa Rais ni ipi?zamani watu waliweza kuishi na wanyama bila tatizo kwa sababu kulikuwa na wakazi 8,000 tu wenye ng’ombe 20 hadi 30., leo hii kuna wakazi 110,000 na mifugo zaidi ya 813,000 wakiwemo ng’ombe, mbuzi na kondoo.” amesema Waziri Mkuu