Ongezeko la Mshahara kuongeza ufanisi kazini

0
243

Mwenyekiti wa chama cha wafanyakazi wa taasisi za elimu ya juu, sayansi, teknolojia, habari, ufundi stadi na utafiti (RAAWU) Taifa, Jane Mihanji amesema ongezeko la mshahara kwa wafanyakazi kwa asilimia 23.3 litaongeza chachu ya ubunifu na ufanisi kazini.

Amesema ongezeko hilo sio tu linakwenda kuboresha mishahara ya wafanyakazi, bali pia litaongeza kiasi cha makato yanayokwenda katika mifuko ya jamii ambayo katika kikokotoo kilichopitishwa kimetaja asilimia 33 kulipwa kwa mkupuo pale mtumishi anapostaafu.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam, Mihanji amesema Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele kuyasikiliza na kuyapatia ufumbuzi masuala mbalimbali ya wafanyakazi, na hivyo kutoa wito kwa waajiri wa sekta binafsi kutambua ongezo hilo.

Amesema RAAWU itaendelea kupigania maslahi bora ya wafanyakazi kwa kukaa pamoja na serikali na waajiri wa sekta binafsi ili kuhakikisha mfanyakazi nchini anakuwa kwenye usalama wa kazi na kufaidi matunda yake wakati anapostaafu.