Nyumba yenye historia ya kusisimua kuhusu maisha ya Mwalimu Nyerere

0
328

Wakati wa Uhai wake, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwahi kuishi katika nyumba hii ikiwa ni baada ya kurejea nchini akitokea masomoni nchin Uingereza.

Huko alihitimu masomo yake na kutunukiwa shahada ya uzamili katika masomo ya uchumi na historia kwenye Chuo Kikuu Cha Edinburgh, akiwa ni mtanzania wa kwanza kusoma chuo kikuu nchini humo.

Licha ya kuitumia nyumba hii akihudumu kwa kazi ya ualimu kwenye shule ya Sekondari Pugu, hapa ndipo palifanikisha kwa asilimia kubwa kutungwa kwa katiba ya TANU.

Mkazi wa nyumba hii kwa sasa ni Mwalimu Andrew Cheyo wa shule ya Sekondari Pugu ambaye anasema akiwa hapa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitumia muda wake wa ziada kukutana na wazee wa chama cha TANU na kuandaa mipango iliyofanikisha kwa kiasi kikubwa kutungwa kwa katiba ya chama hicho.

“Hapa alikuwa anakutana na Wazee waTANU, hatua iliyopelekea kupigwa marufuku na uongozi wa shule wakati ule, na ndipo alipoamua kuwaelekeza Wazee waliokuwa wakija nyumbani kwake nendeni kajiungeni na ofisi iliyokuwa eneo la Pugu na hapo ndipo palipozaliwa Pugu Kajiungeni,” ameongeza Mwalimu Cheyo

Naye Mkuu wa shule ya sekondari Pugu,, Mesajovinus Mutabuzi anasema, ni katika shule hiyo ndipo Mwalimu Nyerere alianzisha sera ya elimu na kujitegemea, ambapo aliwashirikisha Wanafunzi katika kazi mbalimbali za kilimo na ufugaji,

Lakini pia Mwalimu Mutabuzi anasema Mwalimu Nyerere alikuwa karibu na Wanafunzi na alikua akishiriki nao katika michezo na alikua anahakikisha anaelewa mahitaji ya kila Mwanafunzi.

“Mwalimu Nyerere alihakikisha anafundisha somo la ujamaa na kujitegemea kwa vitendo ambapo alihakikisha baada ya kutoka kufundisha darasani pamoja na kusali, alifuatana na Wanafunzi kwenye mafunzo ya vitendo shambani kuangalia mifugo au uwanjani kucheza mpira na wanafunzi.” amesema Mwalimu Mutabuzi na kuongeza kuwa

“Hii ilisababisha Wanafunzi wengi kujua mengi wanayofundishwa darasani na nje ya darasa kwa dhana ya kujitegemea kwa kila kitu.”

Abdul Maulid ni Afisa Elimu wa mkoa wa Dar es salaam na kauli yake ni kuwa, wanaendelea kuhimiza nidhamu, uchapakazi na kuzifahamu falsafa zote za Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ikiwemo ya kupenda kujisomea kwa Walimu na Wanafunzi wa shule ya sekondari Pugu ili alama ya kiongozi huyo mashuhuri iendelee kubaki shuleni hapo.

Kwa Joshua Abraham ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha sita katika shule ya sekondari Pugu na Junior Kazungu wa kidato cha nne, kwao historia ya Baba wa Taifa kufundisha katika shule hiyo inawapa ari ya kusoma kwa bidii ili waje kulitumikia Taifa kama alivyofanya kiongozi huyo..