Zaidi ya nyumba 500 wilayani Rufiji mkoani Pwani zimefunikwa na mafuriko na kusababisha takribani wakazi 3,000 wa wilaya hiyo kukosa makazi.
Mkuu wa Wilaya ya ya Rufiji , Juma Nywayo amesema kuwa mafuriko hayo yamesababishwa na mvua kubwa zilizonyesha wilayani humo na katika maeneo jirani.
Ameieleza kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa wa Pwani iliyotembelea baadhi ya maeneo yaliyokumbwa na mafuriko kuwa, mafuriko hayo pia yamesababisha kukosekana kwa huduma ya umeme kwa kuwa miundombinu mingi ya umeme imeharibiwa, imesababisha kukatika kwa barabara na madaraja, na pia yamezingira Kituo cha Afya cha Muhoro.
Amesema kwa wakazi ambao nyumba zao zimefunikwa kabisa na maji wamehifadhiwa katika kambi za muda ambazo ni Shule ya Sekondari Muhoro na wengine katika Kijiji cha Chumbi.
Baadhi ya wakazi wa Wilaya ya Rufiji ambao nyumba zao zimefunikwa na mafuriko wameiomba serikali iwasaidie kuwahamisha kutoka maeneo ya mabondeni na kuwahamishia maeneo salama.
Akijibu ombi hilo mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama mkoani Pwani ambaye ni mkuu wa mkoa huo Mhandisi Evarist Ndikilo amesema kuwa, wanaandaa utaratibu wa kuwahamishia katika eneo la Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), ambalo miaka ya nyuma serikali ililitoa kwa ajili kuwahamishia wananchi hao lakini walikataa.