Watu watatu wakazi wa kijiji cha Mahurunga wilaya ya Mtwara wamefariki dunia baada ya kushambuliwa na nyati wakiwa shambani.
Kaimu Kamanda wa polisi mkoa wa Mtwara Nicodemus Katembo amesema, watu hao wameshambuliwa hadi kufariki dunia na nyati huyo aliyefika kijijini hapo akitokea porini.
Amesema taarifa za kuwepo kwa nyati huyo zilianza kuwafikia askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wanaolinda mpaka, ndipo walifika haraka kijijini hapo na kumuua.
Kufuatia tukio hilo Jeshi la polisi mkoa wa Mtwara limewataka wakazi wa mkoa huo kutoa taarifa kwenye mamlaka husika pindi wanapoona wanyama wasio wa kawaida katika makazi yao.