NMB yatoa gawio la bilioni 30 kwa serikali

0
121

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango ameagiza mashirika ambayo serikali ina hisa kuhakikisha yanaanza kutoa gawio kwa serikali mara moja.

Pia ameagiza taasisi zinazotakiwa kutoa asilimia 15 ya mapato ghafi kwa mujibu wa sheria zifanye hivyo kikamilifu na kwa wakati.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa hafla ya kupokea gawio la shilingi bilioni 30.7 kutoka benki ya NMB, hafla iliyofanyika jijini Dodoma.

Amesema mashirika ambayo yanategemea ruzuku kutoka mfuko mkuu wa serikali yanapaswa kuwa na mikakati madhubuti na inayotekelezeka ya kupunguza utegemezi kwa serikali na kumuagiza Msajili wa Hazina kuhakikisha wakuu wa taasisi husika wanatekeleza maagizo hayo.

Aidha, Dkt.Mpango amesema serikali itaendelea kuimarisha na kuweka mazingira rafiki na endelevu ya kufanya biashara katika sekta ya fedha na sekta zote nchini.

Ameipongeza benki ya NMB kwa kuendelea kuchangia maendeleo ya jamii, kusaidia ukusanyaji wa mapato ya serikali na kuimarisha mifumo ya ukusanyaji mapato.