Uswisi inatarajia kuanzisha mradi wa majaribio wa kuzalisha umeme kwa kutumia njia za reli kwa kutandaza mitambo ya paneli za sola katikati ya njia hizo, ili kuvuna miale ya jua kwa ajili ya kuzalisha umeme.
Mradi huo unategemewa kugharimu zaidi ya Dola Laki nne na elfu 37 za Kimarekani, ili kutandaza mitambo ya paneli za sola zenye upana wa mita moja ambazo zitawekwa katikati ya reli na paneli hizo zinaweza kuhamishika muda wowote.
Kwa mujibu wa wasimamizi wa mradi huo Sun – Ways, ubunifu huo unaweza kutekelezwa katika nusu ya njia zote za reli duniani na kwamba nafasi katika njia za reli ni pana kuweza kubeba paneli hizo ambazo zina ukubwa wa kawaida bila kuathiri usafiri wa treni zinazotumia njia hizo.
Waanzilishi wa mradi huo wamesema sababu za wao kuja na ubunifu wa aina hiyo ni kuwepo kwa gharama kubwa katika uwekezaji wa mitambo mikubwa zaidi na kukosekana kwa nafasi ya kusimika mitambo hiyo, hivyo wazo la kutumia njia za reli likawa ni mbadala wa changamoto hizo.
Wamesema njia hiyo ni salama na rafiki kwa mazingira.
Ufungaji wa sola paneli katika njia za reli sio jambo geni kwa nchi zilizoendelea, kwani Italia kupitia kampuni ya Greenrail na nchini Uingereza wametekeleza mradi huo ambapo umeme unaozalishwa katika maeneo hayo unatumika kuendesha shughuli za ulinzi na mawasiliano.