Hadi Machi 12, 2020 jumla ya visa vya virusi vya corona vilivyoripotiwa duniani kote ni zaidi ya 129,000 ambapo vifo ni 4,749 na watu waliopona wakiwa ni zaidi ya 68,667.
Virusi hivi vimezidi kusambaa kwa kasi duniani kutokana na urahisi wake wa kuenea ambapo mtu aliyeathirika anaweza kumuambukiza mwenzake akikohoa au kupumua na kurusha matone ya mate ambayo yanakuwa na virusi hivyo.
Katika maeneo ya kazi, mate hayo yakidondoka kwenye meza, laptop, tablets na ukiyagusa kwa mikono na kisha ukagusa uso wako (macho, pua, mdomo), maambukizi yanaenea zaidi.
Kutokana na hatari hiyo, hizi ni njia sita rahisi za kujikinga virusi hivyo;
- Safisha eneo la kazi
Safisha vifaa vyako vya kazi kama vile meza, laptops, viti kwa kutumia dawa maalum (disifectant) za kuua vijidudu. Pia safisha vitu vingine unavyovishika mara kwa mara kama vile simu, mouses ili kuhakikisha unadhibiti maambukizi. - Weka visafishia mikono (sanitisers) kila mahala
Hakikisha kuwa unaweka sanitisers za kusafishia mikono kwa ajili ya kuua vijidudu kila mahala katika maeneo ya kazi, ili kuhakikisha kuwa mikono inakuwa salama kila wakati. - Safisha mikono yako mara kwa mara
Hii isiwe kwako tu, bali pia himiza wafanyakazi wenzako kufanya hivyo kwani mikono yako pekee ikiwa safi, na wengine ikawa michafu, bado utakuwa kwenye hatari kubwa ya kuweza kupata maambukizo. - Kaa mbali na waathirika
Shirika la Afya Duniani (WHO) linashauri kukaa umbali wa angalau mita moja kutoka kwa mtu anayekohoa, ili kuepuka kurushiwa matone ya mate ambayo hubeba vijidudu. - Fanyia kazi nyumbani inapohisi unaumwa
Shirika la Afya Duniani (WHO) linashauri mtu yeyote anayekohoa au mwenye homa afanyie kazi nyumbani ili kuhakikisha anaepusha kuwa karibu na watu wengine na kusababisha maambukizi zaidi. - Funika mdomo unapokoa
Unapopiga chafya, unapokohoa hakikisha kuwa unafunika mdomo na pua ili kuhakikisha hauathiri watu wengine waliopo jirani na wewe.
Inapohisi kuwa na dalili za ugonjwa wa COVID-9 inatakiwa kujitenga na kuangalia kwa karibu afya yako kwa siku 14 huku ukipima joto la mwili mara mbili kwa siku. Endapo utaona hali yako inazidi kuwa mbaya nenda hospitali, hasa kama umetoka katika nchi au eneo ambalo limeathiriwa na virusi hivyo.